Emmanuel Martin (kushoto) akishangilia pamoja na Obrey Chirwa aliyembeba Simon Msuva baada ya kuifungia Yanga bao katika moja ya mechi za Ligi Kuu msimu uliopita kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
|
MSHAMBULIAJI wa Yanga, Emmanuel Martin amevalishwa viatu vya Simon Msuva katika timu ya taifa, Taifa Stars iliyokusanyika kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Botswana Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga amemchukua mshambuliaji huyo kwa kuwa ameonesha kiwango kizuri katika mechi mbili za mwanzoni mwa msimu huu ambapo Yanga ilicheza na Simba mkicha Lipuli FC katika Ligi Kuu na michezo ya kirafiki.
Kama alivyo Msuva, Martin amekuwa akicheza kwa kujituma wakati mwingine akirudi hadi nyuma kusaidia ulinzi kucheza kati katika pamoja na wingi ya kulia na kushoto.
Mayanga, amechukua uamuzi wa kumwita nyota huyo baada kuna uwezekano akawakosa Msuva anayecheza soka la kulipwa timu ya Difaa El Jadidah ya Morocco na Orgenes Mollel wa FC Famalicao ya Ureno, kutokana na taratibu za kupata viza zimekuwa na mlolongo
Martin alijiunga na kambi ya Taifa Stars jana na kuanza na mazoezi na wenzake kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Wachezaji wa kimataifa wengine wa tanzania wanaocheza soka nje walioripoti ni Mbwana Samatta (KRC Genk/Ubelgiji), Elias Maguli (Dhofar FC/Oman), Abdi Banda (Baroka FC/Afrika Kusini), Hamis Abdallah (Sony Sugar/Kenya) wakati Farid Mussa wa CD Tenerif ya Hispania alitarajiwa kutua jana.
Wachezaji walioitwa kwenye timu hiyo ni makipa, Aishi Manula (Simba SC), Mwadini Ally (Azam FC) na Ramadhani Kabwili (Yanga).
Walinzi ni Gadiel Michael (Yanga), Boniface Maganga (Mbao FC), Kelvin Yondani (Yanga), Salim Mbonde (Simba SC) na Erasto Nyoni (Simba SC).
Viungo ni Himid Mao (Azam FC), Mzamiru Yassin (Simba SC), Said Ndemla (Simba SC), Shiza Kichuya (Simba SC) na washambuliaji ni Raphael Daud (Yanga) na Kelvin Sabato (Azam FC).
Katika benchi la ufundi pamoja na Kocha Mayanga wengine ni, Fulgence Novatus (Kocha Msaidizi), Patrick Mwangata (Kocha wa Makipa), Danny Msangi (Meneja), Dkt. Richard Yomba (Daktari wa timu), Dkt. Gilbert Kigadye (Daktari wa Viungo) na Ally Ruvu (Mtunza Vifaa).
Comments
Post a Comment