NEW YORK, Marekani
MSHAMBULIAJI Neymar Santos, ameutia nguvu uvumi wa kuondoka katika timu ya Barcelona baada ya kukaa kwa dakika takribani 15 kwenye chumba cha kubadilishia jezi cha Real Madrid baada ya kuisha mchezo ambao Barcelona ilishinda mabao 3-2 mjini Miami, Marekani.
Mchezaji huyo wa Brazili, amekuwa akihusishwa na kuhamia timu ya Paris Saint-Germain kwa ada ya pauni milioni 196 ambayo imo kwenye kipengele cha mkataba wake kama kuna timu inataka kuuvunja na kumchukua.
Baada ya kuisha mchezo huo wa Jumamosi, alibadilishana jezi na Sergio Ramos na Casemiro na kuonekana kama vile alikuwa akiagana na rafiki zake, taarifa nchini Hispania zimesema .
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 25, pia alionekana akiwa pamoja na mshambuliaji wa zamani wa Real Madrid na Brazil, Julio Baptista baada ya mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Hard Rock.
Neymar alitoa pasi mbili za mabao katika mchezo huo wa El Clasico ambao unaweza kuwa mwisho kwake kama atahama huku Lionel Messi, Ivan Rakitic na Gerard Pique wakifunga mabao kwa timu yao inayonolewa na kocha Ernesto Valverde.
Mlinzi wa Madrid, Ramos amesema kuwa kama Neymar ataondoka inaweza kuwa kitu kizuri kwa timu yake na kocha wao, Zinedine Zidane.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo kuhusu Neymar, Ramos alisema, ''Sijui kila mmoja yuko huru kuchagua kuhusu hatima yake ya baadaye. Ninatumaini (kama atahama) itakuwa ni tatizo dogo kwetu.''
Kocha Valverde kwa upande wake alisema baada ya mchezo kwamba anatumaini Neymar kubakia Barcelona na waataanza naye msimu mpya wa La Liga mwezi huu.
Wakati huohuo, habari nyingine zinasema kuwa Neymar huenda akapimwa afya katika timu ya Paris Saint-Germain wiki hii.
Comments
Post a Comment