ROMA, Italia
RIYAD Mahrez kesho atafanyiwa vipimo kabla ya kusaini mkataba wake wa pauni milioni 31.3 katika timu ya Roma, habari kutoka Italia zimesema.
Mchezaji huyo Bora wa Chama cha Wachezaji wa Kulipwa England (PFA) 2015-16 ameiambia timu yake ya Leicester kwamba anataka kuondoka ili kuendeleza kipaji chake.
Gazeti la Corriere dello Sport ambalo linajulikana kuwa karibu na timu hiyo ya Giallorossi limesema klabu zote mbili zimefikia makubaliano kuhusu ada huku Leicester maarufu kama 'Foxes’ (mbweha) ikitaka kumsaini Kelechi Iheanacho kutoka Manchester City kama mrithi wa Mahrez.
Mahrez baada ya kutua mjini Roma, leo anatarajiwa kupimwa afya kabla ya kusaini mkataba mpya kwa miamba hiyo ya Serie A.
Arsenal na Tottenham ni timu nyingine zilizokuwa zikimsaka mchezaji huyo raia wa Algeria, lakini zilikwazwa na ada iliyokuwa ikitakiwa na timu yake.
Roma ikiwa chini ya Mkurugenzi wa soka, Monchi imekuwa ikisaini wachezaji kujiimarisha baada ya kuondoka kwa Thomas Vermaelen, Wojciech Szczesny, Antonio Rudiger na Mohamed Salah huku pia ikitarajia kumuuza Kostas Manolas.
Mahrez mwenye umri wa miaka 26 anatarajiwa kuwa mrithi wa Salah, aliyesainiwa na Liverpool baada ya kufunga mabao 19 msimu uliopita.
Mahrez akiwa na Mbweha katika msimu wa 2015-16 ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu England na kuisaidia timu yake kufika robo fainali katika Ligi ya Mabingwa.
Comments
Post a Comment