Kuwaona Mayweather, McGregor laki 290
NEW YORK, Marekani
EDDIE Hearn amesema bondia Floyd Mayweather anataka mashabiki wa Uingereza kulipa pauni 100 (zaidi ya sh. 290,000) kwa kila mtu ili kuona katika televisheni pambano lake dhidi ya Conor McGregor, lakini kituo cha Sky kinataka iwe pauni 19 (zaidi ya sh. 55,000).
Huku zikiwa zimesalia wiki nne, mashabiki bado hawajatangaziwa rasmi kuhusu ni kiasi gani watalipia ili kuona moja kwa moja pambano hilo kwenye runinga na ni kituo gani kitarusha.
Eddie Hearn ambaye ni kocha wa masumbwi, amesema anahisi Mayweather atachaji kiasi hicho cha fedha kwa pambano lao litakalofanyika Agosti 26, mwaka huu mjini Las Vegas.
Wakati wa pambano kati ya Mayweather dhidi ya Manny Pacquiao mwaka 2015, kiasi cha juu cha kuona pambano hilo ilikuwa ni dola 89.99 (zaidi ya sh.200,000 na dola 99.99 (zaidi ya sh 220,000.
Katika mahojiano kati ya Eddie Hearn na GQ alisema Mayweather anapenda kiasi cha kuonesha pambano hilo katika runinga kuwa pauni 100, Uingereza kiwango ambacho kama kitatangazwa kitakuwa kikubwa zaidi, cha kawaida ni wastani wa pauni 15 (zaidi ya sh.40,000).
Wakati huohuo, mauzo ya tiketi za mchezo huo yameendelea kusuasua kutokana na kinachooonekana kiingilio chake kuwa kikubwa.
Hadi kufikia Jumamosi mamia kwa maelfu ya viti vya uwanja wa T-Mobile vilikuwa bado havijapata watu kutokana na tiketi zake kutonunuliwa.
Bei ya tiketi inafika hadi pauni 2,665 (ambazo ni zaidi ya sh. milioni 7 za Tanzania), inawezekana mashabiki wanasubiri kama inaweza kupungua.
Hata hivyo promota Leonard Ellerbe haonekani kuwa na wasiwasi anasema anatumini zitanunuliwa na mapato yake kuvunja rekodi.
Mapato katika pambano kati ya Mayweather dhidi ya Pacquiao mwaka 2015 yalikuwa pauni 54,974,873 (zaidi ya sh. bilioni 161) ikiwa ni makubwa mara tatu zaidi ya mapato makubwa yaliyowahi kutokea.
Viti vya karibu na ulingo kiingilio chake ni pauni 7,600 (zaidi ya milioni 22) huku tiketi viti vingine vya karibu zaidi vikilipiwa kwa pauni 11,417 (zaidi ya sh. milioni 33)
Comments
Post a Comment