MADRID, Hispania
MWANASOKA nyota Cristiano Ronaldo leo ametinga katika mahakama nchini Hispania ambako anakabiliwa na mashitaka ya kukwepa mamilioni ya kodi .
Waendesha mashtaka wanamtuhumu Ronaldo ambaye ni manamichezo mwenye mapato makubwa zaidi duniani kukwepa kodi ya takribani dola milioni 17.3 (zaidi ya sh, bilioni 38.7).
Alitarajiwa kusema chochote baada ya kusomewa mashitaka lakini haikuwa hivyo.
Nyota huyo wa Real Madrid mwenye umri wa miaka 32, awali alikanusha tuhuma hizo kwa kusema kuwa yeye ni mtu safi.
Ronaldo ni mwanasoka wa mwisho katika msururu wa wanasoka walioshitakiwa na mamlaka ya kodi ya Hispania.
Nyota wa Argentina, Lionel Messi, anayeichezea Barcelona, alihukumiwa kifungo cha miezi 21 baada ya kukutwa na hatia ya kukwepa kodi mwaka jana.
Mwanzoni mwa mwezi huu, mahakama ilisema anaweza kulipa euro 252,000 (zaidi ya sh. milioni 661.6) ili asifungwe.
Ronaldo alikaa mahakamani kwa muda wa saa moja na nusu, alitoa ushahidi kwa majaji wa mahakama ya Pozuelo de Alarcón iliyopo nje kidogo ya mji wa Madrid.
Waandishi wa vyombo vingi vya habari walikuwepo mahakamani kusubiri kumwona na kumpiga picha Ronaldo, lakini hawakuambulia kitu kutokana kuingia kwa kupitia njia ya chini inatokea gereji.
Wakati wa kutoka, Ronaldo alitarajiwa kuzungumza chochote lakini aliondoka kwenda nyumbani kwake moja kwa moja na kufanya baadhi ya waandishi kumzomea.
Kwa mujibu waendesha mashitaka, Ronaldo alikwepa kodi hiyo kwa kutumia muundo wa kampuni aliyoianzisha 2010 kuficha mapato yake na kodi aliyotakiwa kulipa nchini Hispania yanayotokana na haki za kutumika kwa picha yake, kitu ambacho kinyume cha sheria.
Uongozi wa Ronaldo nao umekanusha madai hayo.
Akikutwa na hatia mshambuliaji huyo raia wa Ureno anaweza kutowa faini ya euro milioni 28 na kifungo cha miaka mitatu na nusu.
Comments
Post a Comment