Mwandishi wetu
KAMPUNI ya Michezo ya Kubashiri nchini, SportPesa imepiga jeki timu ya Polisi Tanzania kwa kutoa msaada wa sh. milioni 20 na vifaa ili kujiandaa kwa Ligi Daraja la Kwanza inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Msaada huo umepokewa jana Dar es Salaam na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro ambaye ameishukuru SportPesa kuutoa kwa wakati mzuri na utasaidia katika maandalizi.
“SportPesa ni wadau wetu na ni wadau welevu, wameona umuhimu wa kuchangia fedha na vifaa vya michezo kwa timu ya Polisi, hii itatusaidia sana. “Naahidi kwamba fedha hizo tutazitumia vizuri kujiandaa kwa ajili kupanda na kuingia Ligi Kuu kwa moto mkali na kuhakikisha kuwa tunaleta heshima kwa Jeshi la Polisi na wafadhiri wetu mliotupatia vifaa vyetu leo,” alisema IGP Sirro.
Akizungumza katika hafla hiyo, mkurugenzi wa utawala na utekelezaji Wa SportPesa, Tarimba Abbas alisema: “Tunatambua mchango wa timu ya polisi Tanzania kwa Jamii kiujumla kwani wanafanya kazi kubwa kuhakikisha sheria za nchi zinafuatwa bila kuvunjwa.
“Kampuni ya SportPesa inatoa kiasi cha Mil.20 na jezi kwa timu ya Polisi Tanzania ambazo zitatumika katika shughuli mbalimbali ili kuimarisha timu hiyo kwani tumedhamiria kuendeleza na kukuza mpira wa miguu nchini kwa kutoa msaada kwa timu mbalimbali,” alisema Tarimba.
Pia, SportPesa ilikabidhi cheti cha kutambua mchango kwa Jeshi la Polisi kutokana na kusimamia ulinzi na usalama hasa wakati wa ziara ya Klabu ya Everton hapa nchini Julai mwaka huu, kucheza na Timu ya Gor Mahia ya Kenya.

Comments
Post a Comment