![]() |
| Sadio Mane (kulia) akiwa na Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp. |
LONDON, Uingereza
TIMU ya Liverpool imeshindwa katika rufaa yake iliyokata kupinga adhabu ya kufungiwa mechi tatu kwa Sadio Mane baada ya kuoneshwa kadi nyekundu Jumamosi katika mchezo wa Ligi Kuu England baada ya kumchezea vibaya mlinda mlango wa Manchester City, Ederson.
Katika mchezo huo ambao Liverpool ilifungwa mabao 5-0, Mane alitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 37 baada ya kunyanyua mguu na kumgonga Ederson usoni.
Baada ya kutupwa kwa rufaa hiyo, sasa Mane atakosa mechi za Ligi Kuu dhidi ya Burnley na Leicester, na mchezo mwingine wa Kombe la Ligi.
Kuhusu suala la kuongezewa adhabu, lilitupwa na kamisheni huru inayoshughulika kusikiliza rufaa.
Awali baada ya kuisha mchezo huo Jumamosi, Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp alisema si yeye wala kocha mwenzie wa City, Pep Guardiola hakuna aliyefikiria mwamuzi angetoa adi nyekundu kwa Mane.
Wachambuzi wa soka Alan Shearer, Gary Lineker na Ian Wright walisema wachezaji wote walikwenda kucheza mpira, huku Chris Sutton akisema kuwa kadi nyekundu ya Mane inatakiwa kufutwa.
Shearer alisema kadi nyekundu itaendelea kuwa hivyo kulingana na sheria za sasa. Mchezaji wa zamani wa England, Jamie Carragher na Phil Neville ni miongoni mwa wachambuzi waliosema kuwa refa Jon Moss alikuwa sahihi kumwonesha kadi Mane.
Ederson alifanya mazoezi jana wakati City ikijiandaa kwa mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Feyenoord.

Comments
Post a Comment