![]() |
| Uwanja wa Azam Complex |
Mwandishi wetu
TIMU ya Azam FC imefurahia uamuzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuwaruhusu kuutumia uwanja wao wa Azam Complex uliopo Chamazi kwa mechi zake zote za nyumbani za Ligi Kuu Tanzania ikiwemo dhidi ya Yanga na Simba .
Kwa mara ya kwanza vigogo vya soka nchini, Yanga na Simba zitacheza katika uwanja wa Azam Complex, unaomilikiwa na Azam FC, iliyoanzishwa mwaka 2007.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Meneja wa Azam FC, Philipo Alando alisema wamefurahia kupata fursa ya kuutumia uwanja wao wa nyumbani kitu walichokuwa wanakililia.
“Ni jambo jema, tunafurahi kuona TFF hii inatoa makandokando yote ambayo yalikuwa magumu kufanyika huko awali, kama kuruhusu uwanja huu wa Chamazi kutumika kwa michezo yote.
Mabingwa wa Ngao ya Jamii, Simba ndio watakuwa wa kwanza kuandika historia ya kucheza na Azam FC kwenye uwanja huo katika mchezo wa Ligi Kuu ta Vodacom, Jumamosi hii.
Kwa upande wa mabingwa watetezi ligi hiyo, Yanga itashuka Chamazi Complex kuwavaa Azam katika mchezo wa mwisho wa kufunga mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, Desemba 29 mwaka huu.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya kikosi kazi, kilichopewa kazi maalumu ya kupitia upya ratiba iliyokuwa imeandaliwa awali kuifanyia marekebisho, kumaliza majukumu kazi yake juzi na kutoa ratiba mpya inayoonesha uwanja huo kuanza kutumika kwa michezo mikubwa na miamba hiyo.
Uamuzi huo umefanywa na uongozi mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), ulioingia madarakani Oktoba 12, mwaka huu tofauti wa awali uliotoa msimamo kuwa timu za Simba na Yanga zina mashabiki wengi hivyo uwanja huo ni mdogo (unaingiza mashabiki wachache 7,000) hivyo kutokuwa salama.

Comments
Post a Comment