![]() |
| Robin van Persie |
AMSTERDAM, Uholanzi
KOCHA wa Uholanzi, Dick Advocaat amemwita tena kwenye kikosi cha timu yake mshambuliaji mkongwe, Robin van Persie kwa ajili ya kuunganika na wenzie kwa ajili ya kujiandaa kwa michezo miwili ya kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Dunia Urusi mwakani, dhidi ya Ufaransa na Bulgaria.
Nyota huyo wa Fenerbahce kwa mara ya mwisho aliichezea timu yake ya Taifa Oktoba 2015 ameshaichezea mechi 101.
Mchezaji huyo wa zamani wa Arsenal mwenye umri wa miaka 34 ambaye aliwahi pia kuichezea Manchester United ana rekodi ya kufunga mabao mengi kuliko mchezaji yeyote katika timu ya Uholanzi akiweka kimiani mabao 50.
"Bado ninafikiria ni mmoja wa washambuliaji mahiri ambao tunao,'' Advocaat alisema wakati akitangaza kikosi chake na kuongeza anaamini anaweza kutoa mchango muhimu kwa timu ya Uholanzi.
Van Persie ni mmoja kati ya washambuliaji waliojumuishwa katika kikosi sanjari, Memphis Depay wa Lyon na mshambuliaji wa Tottenham, Vincent Janssen.
Baada ya kucheza mechi sita, Uholanzi iko katika nafasi ya tatu kwenye Kundi A, inazidiwa pointi tatu nyuma na Sweden inayoongoza kundi kwa tofauti ya mabao na Ufaransa.
Timu zitakazoshinda mechi za mwisho pekee ndizo zitafuzu michuano ya Kombe la Dunia.
Wachezaji wengine wakongwe waliojumuishwa na kocha huyo kwenye kikosi cha wachezaji 24 pamoja na Van Persie ni nahodha Arjen Robben na kiungo Wesley Sneijder.
Kikosi kamili kilichoitwa ni:
Makipa: Jasper Cillessen (Barcelona), Maarten Stekelenburg (Everton) na Jeroen Zoet (PSV Eindhoven)
Walinzi: Nathan Ake (Bournemouth), Daley Blind (Manchester United), Wesley Hoedt (Southampton), Matthijs de Ligt (Ajax), Karim Rekik (Hertha Berlin), Kenny Tete (Olympique Lyon), Joel Veltman (Ajax) na Stefan de Vrij (Lazio).
Viungo: Donny van de Beek (Ajax), Marco van Ginkel (PSV), Tonny Vilhena (Feyenoord), Davy Proepper (Brighton & Hove Albion), Wesley Sneijder (Nice), Kevin Strootman (Roma) na Georginio Wijnaldum (Liverpool).
Washambuliaji: Memphis Depay (Olympique Lyon), Bas Dost (Sporting Lisbon), Vincent Janssen (Tottenham Hotspur), Robin van Persie (Fenerbahce), Quincy Promes (Spartak Moscow) na Arjen Robben (Bayern Munich).

Comments
Post a Comment