![]() |
| Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia (kulia) akiwa na makamu wake Rais, Michael Wambura. |
RAIS wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (Fifa), Gianni Infantino, ametuma salamu za pongezi kwa shirikisho la Tanzania (TFF), Wallace Karia kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa TFF kwa kipindi cha miaka minne ijayo ya 2017-2021.
Taarifa ya TFF iliyotolewa na Ofisa habari wake, Alfred Lucas ilisema Infantino amempongeza Karia na viongozi wenngine kwa barua maalumu.
Katika barua yake hiyo ya Agosti 14, 2017 aliyoiandika kutoka Zurich, amesema: “Ningependa kuchukua nafasi hii kukupa pongezi zangu dhati. Nakutakia kila la kheri katika majukumu yako.”
![]() |
| Rais wa Fifa, Gianni Infantino |
Amesema hana shaka na uwezo wa Karia hasa ikizingatiwa kuwa alikuwa Makamu wa Rais wa kipindi kilichopita, hivyo atakuwa fursa thabiti ya kuiletea nchi maendeleo ya mchezo soka.
“Kwa wakati wote, nakuhakikishia ushirikiano wa kutosha kutoka Fifa katika malengo yako. Milango ya Fifa iko wazi wakati wowote wewe kuja kujadili masuala ya mchezo wa mpira wa miguu hasa eneo la utawala.
“Ningependa kuchukua nafasi hii kukualika kuja hapa Zurich (Uswisi) wakati wowote kuanzia sasa ambako nitapata fursa ya kukutambulisha maeneo mbalimbali ya Fifa. Nimeagiza upande wa utawala kuwasiliana nawe kuona na kupanga tarehe rasmi ya safari,” amesema na kuongeza:
“Nikutakie tena kheri na fanaka, nguvu na kila aina ya mafanikio katika majukumu yako mapya huku nikitarajia ujio wa kuonana nawe haraka.”
Wakati huo huo, Shirikisho la Mpira wa Miguu la Rwanda (FERWAFA) kupitia Rais wake,Nzamwita Vincent nalo kwa upande wake wamempongeza Rais wa TFF, Wallace Karia kwa kuchaguliwa kuwa kiongozi mpya wa shirikisho.
FERWAFA imesema kwamba Rwanda itaendelea kuwa bega kwa bega na Tanzania katika maendeleo ya mpira wa miguu kwa ushirikiano baina ya nchi mbili kadhalika ukanda wa Afrika Mashariki unaounda Baraza la Sola la nchi za Afrika Mashariki.


Comments
Post a Comment