![]() |
| Neymar |
PARIS, Ufaransa
TIMU ya Paris Saint-Germain imekana kufanya kosa lolote katika kumsaini Neymar Santos Jr kutoka Barcelona na kusema inashangazwa msimamo wa klabu hiyo kutaka kuchukua hatua ya kisheria dhidi ya nyota huyo ikidai amevunja masharti ya mkataba.
Jumanne, Barca ilitangaza itamshitaki Neymar kutaka kurudishiwa kiasi cha fedha ilichomlipa baada ya kusaini kuongeza mkataba wake Oktoba mwaka jana pamoja na kutaka fidia ya euro milioni 8.5 na asilimia 10 nyingine kwa kuchelewesha malipo".
Barca pia imesema kama Neymar hatalipa, wanatarajia PSG itawajibika.
Neymar alihamia PSG ambayo ilitumia kifungu cha mkataba wake kinachoelekeza kutolewa kiasi cha pauni milioni 199 ( zaidi ya sh. bilioni 570).
Wakati Neymar aliifungia timu yake mpya mabao mawili Jumapili iliopita katika mchezo wake wa kwanza, bodi ya Barcelona imesema itachukua hatua, PSG imekana kufanya kosa lolote kwa upande wao au ule wa mchezaji wao.
"Paris Saint-Germain ilishangazwa na kuona taarifa ya FC Barcelona leo ikisema kwamba inaanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mchezaji wao wa zamani Neymar Jr na kusema kama Neymar Jr atashindwa kulipa fedha zinazodaiwa na klabu yake ya zamani, Paris Saint-Germain itatakiwa kulipa kiasi chote.
"Paris Saint-Germain inasema tena kwamba, kama ilivyo kwa Neymar Jr, imekuwa ikiheshimu kanuni na sheria zote katika kuingia mikataba na kwa mara nyingine, tunasikitishwa na inavyofanya FC Barcelona," imesomeka taarifa ya PSG.

Comments
Post a Comment