| Frederick Mwakalebela alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari (hawako pichani) Dar es Salaam leo |
Watatu hao wamefanya mikutano yao na waandishi wa habari, iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam, kila mmoja akiwashawishi wajumbe kuwapa nafasi ili kufanya vizuri katika uongozi na kuleta maendeleo ya soka
Mwakalebela aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa (TFF), amesema akiingia madarakani atahakikisha kamati zitakazoteuliwa zitakuwa huru,atahakikisha zinafanya vikao vyake na kuzingatia kanuni, sheria na taratibu zilizowekwa, kuzingatia misingi ya utawala bora na kuhakikisha programu za maendeleo za timu za taifa za wanawake, wanaume, vijana na ufukweni zinafanyika ili kumaliza tatizo la kutofanya vizuri katika mashindano .
Pia amesema suala la mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara kuwa na viporo halitakuwapo vile vile ataimarisha uhusiano na wadau wa mchezo huo hasa serikali.
Naye Mayai anayewania nafasi hiyo iliyoachwa wazi na Jamal Malinzi amewaomba wajumbe kuchagua ili aweze kuleta mabadiliko ya uendeshaji wa soka .
Amesema akipata nafasi hiyo atashirikiana na wajumbe kukuza kiwango cha soka na kutoa mfano wanawake wamekuwa wakifanya vizuri kwa sababu ya kushiriki katika mashindano mbalimbali.
Mayai aliyeandamana na wachezaji wa zamani akiwamo Zamoyoni Mogella, Khalid Mohamed, Lawrence Mwalusako na Aaron Nyanda ametaja vipaumbele vyake vingine ni kusimamia mpira wa miguu vizuri kuanzia ngazi ya vijana, wanawake na ngazi ya juu kwa weledi.
Naye Katibu Mkuu wa Mbeya City Emmanuel Kimbe, ambaye naye anawania nafasi hiyo ya juu amesema atahakikisha mchezo wa soka unarejesha heshima yake kama ilivyokuwa miaka ya nyuma huku akiahidi kupambana kuboresha miundo mbinu ambayo sasa iko katika hali moja.
Mgombea Urais wa TFF, Imani Madega akizungumza na waandishi wa habari leo wakati akizindua rasmi kampeni yake ya Uchaguzi wa unaotarajiwa kufanyika Jumamosi hii, Dodoma.
Imani Madega, Mwenyekiti wa zamani wa Yanga, amesema kuwa anaamini ana uwezo wa kuiongoza TFF kwa kuheshimu sheria na kusimamia uadilifu kama alivyofanya akiwa anaiongoza Yanga na kuacha kiasi cha Sh. milioni 200 wakati anaondoka madarakani.
Uchaguzi wa TFF unatarajiwa kufanyika keshokutwa mjini Dodoma na tayari wajumbe na wagombea wameshafika mkoani humo kuendelea kujinadi kwa wapiga kura.

Comments
Post a Comment