BERLIN, Ujerumani
KOCHA wa Liverpool, Jurgen Klopp ameipiga kijembe Barcelona kwa kuiambia ihifadhi nguvu zake wakati ambapo inaendelea kuhusishwa na kumtaka kiungo wao mshambuliaji
Philippe Coutinho.
Coutinho usiku wa kuamkia leo aliisaidia Liverpool kupata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya mabingwa wa Bundesliga, Bayern Munich katika mchezo wa Kombe la Audi, itacheza fainali leo dhidi ya Atletico Madrid, huku bayern ikianza kucheza dhidi ya Napoli kusaka mshindi wa tatu.
Mchezaji huyo wa Brazil mwenye umri wa miaka 25, anawindwa na miamba ya LaLiga, Barcelona, ikitaka kumfanya kama mrithi wa Neymar, ambaye anaonekana kama anaweza kutimkia Paris Saint-Germain.
Klopp amesisitiza kuwa Coutinho hauzwi, na kuiambia Barca isipoteze muda wake kumfutilia.
" Ninaweza kuelewa kuwa Coutinho ana kiwango kikubwa sana, lakini wanaweza kuhifadhi nguvu zao," aliwaambia waandishi wa habari.
Klopp alifurahia kiwango cha Coutinho, aliyeanza kucheza katikati kabla ya kuhamia kushoto katika mchezo dhidi yaBayern.
Mabao yaliofungwa na Sadio Mane, Mohamed Salah na Daniel Sturridge yaliifanya Liverpool kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Bayern katika uwanja wa Allianz Arena.

Comments
Post a Comment