![]() |
| Cosmas Kapinga (kulia) |
Mwandishi wetu
KAMATI ya Utendaji ya klabu ya Simba imemteua aliyewahi kuwa daktari wa klabu hiyo, Cosmas Kapinga kuwa Meneja mpya wa timu yao ya soka inyoshiriki Ligi Kuu
Ofisa Habari wa klabu hiyo, Haji Manara alisema Dar es Salaam jana kuwa Kapinga anachukua nafasi ya Mussa Hassan Mgosi aliyepangiwa majukumu mengine ndani ya klabu.
Alisema Kapinga ataanza kazi yake mpya, mara baada ya kikosi cha Simba kurejea nchini kutoka Afrika Kusini, ilikoweka kambi kwa maandalizi msimu mpya.
Kuhusu Mgosi, alisema atakuwa kocha msaidizi na meneja wa timu ya vijana, sambamba na Nico Nyagawa ambaye atakuwa kocha msaidizi wa kikosi hicho, huku pia akiwa mratibu chini ya kocha mkuu Nico kiondo.
Mgosi anatarajiwa kupewa mafunzo ya ukocha leseni C, ikiwa ni hatua ya kuongeza ujuzi kwenye majukumu mapya ya ukocha katika timu ya vijana.
Wakati huo huo, benchi la ufundi la timu ya Simba limesema limeridhishwa na maandalizi yao Afrika Kusini, na jinsi timu ilivyocheza vizuri na Orlando Pirates juzi, licha ya kufungwa bao 1-0.
Leo timu hiyo itashuka kwenye Uwanja wa Sturrock Park uliopo ndani ya Chuo kikuu cha Wits, Johannesburg kucheza mechi ya mwisho ya maandalizi nchini humo dhidi ya Bidvest, ambao mabingwa wa Afrika Kusini kwa sasa.

Comments
Post a Comment