PARIS, Ufaransa
NEYMAR ameshindwa kucheza mechi yake ya kwanza katika timu ya Paris Saint-Germain kutokana na kuwepo dosari katika nyaraka za kumwezesha kufanya kazi, zilizotayarishwa na mamlaka za soka za Hispania na Ufaransa.
PSG ilimtambulisha mchezaji huyo ghari zaidi duniani kwa vyombo vya habari Ijumaa iliyopita baada ya kukamilisha uhamisho Alhamisi kwa ada iliyoweka rekodi mpya ya usajili ya pauni 200 (zaidi ya sh. bilioni 589) akitokea Barcelona ya Uhispania, amesaini mkataba wa miaka mitano.
Kiasi cha fedha kilichotumika kama ada ya kumnunua inaweza kununua ndege tatu kubwa za abiria 175 aina ya Boeing 737-700 ambapo kila moja inauzwa dola milioni 82.4 (zaidi ya sh. bilioni 184.4) kila moja.
Neymar katika utambulisho wake alisema yuko fiti na kuwa tayari kuanza kucheza katika timu ya Parc De Princes katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Ufaransa dhidi ya Amien leo.
Hata hivyo, taarifa kutoka Ufaransa zinasema Shirikisho la Mpira wa Miguu Ufaransa, Bodi ya Ligi ilihitaji Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) wa mchezaji huyo Ijumaa ili kumruhusu acheze mchezo leo jioni.
Hadi kufikia Ijumaa usiku, LFP haikupata nyaraka kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu la Hispania.
Inafahamika Maofisa wa La Liga hawajafurahi uhamisho wa wa Neymar huku Rais Javier Tebas akisema shirikisho litatuma malalamiko kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA) na kudai kuwa klabu ya Ufaransa (PSG) ni ya 'fedha za madawa''.
''Malalamiko tayari na yatawasilishwa kwa UEFA, Umoja wa Ulaya na Mahakama ya Uswisi ,'' alisema Tebas.
'' Kimsingi, malalamiko yanahusu ushindani usiokuwa wa haki na dhidi ya timu ambazo zinaongezewa fedha na wamiliki wake kwa kutoa zawadi ya wachezaji kwa mashabiki wao. PSG ni mfano mzuri wa 'fedha za madawa' aliongeza Tebas.
''Akaunti za PSG zinaonesha kwamba ina mapato makubwa kuliko Real Madrid au Manchester United, kitu ambacho kinamaanisha kwamba thamani ya brand yao ni kubwa kuliko klabu hizo mbili . Sawa, hiyo inawezekana,'' alisema
Awali Naymar alitarajia kujumuishwa jana katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu wa PSG dhidi ya timu ya Amiens ambayo imepanda daraja msimu huu, siku moja tu baada ya kutambulishwa kama mchezaji mpya.
Neymar amecheza kwa mafanikio misimu minne Nou Camp baada ya kujiunga akitokea Santos mwaka 2013 , ametwaa nayo makombe mawili La Liga , vikombe vitatu vya Copa del Reys na kimoja cha Ligi ya Mabingwa.
Amejiunga na PSG ambayo katika msimu uliopita ilishika nafasi ya pili katika ligi ikipokwa ubingwa na Monaco, yenyewe ilitwaa Kombe la Ufaransa na Kombe la Ligi Ufaransa.
Mmiliki wa timu ya PSG, Nasser Al-Khelaifi amesema melango yake ni kuona wanatwaa taji la Ligi ya Mabingwa baada ya msimu uliopita kutolewa katika hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Barcelona huku Neymar aking'ara kwenye mchezo wa marudiano baada ya kuwa chini kwa mabao manne katika mchezo wa kwanza.

Comments
Post a Comment