Mwandishi Wetu
BONDIA
wa ngumi za kulipwa nchini, Cosmas Cheka amekata rufaa Baraza la Michezo la
Taifa (BMT) kupinga matokeo, adhabu ya kufungiwa miezi sita na faini ya Sh. 200,000
iliyotangazwa na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC).
Cheka
alisema hayo jana kwenye mkutano na waandishi wa habari na kusema TPBC ilikuwa na njama dhidi yake ili
kumtengenezea nafasi bondia Haidary Mchanjo katika ngumi za kulipwa nchini.
Alifafanua,
adhabu dhidi yake haikufuata sheria kwani kwanza hakupewa nafasi ya kusikilizwa
kwa mujibu wa sheria, huku TPBC ikimpa nafasi mwamuzi wa pambano hilo, Modest
Rashid aliyetaka kupigana naye kujieleza
katika kikao cha TPBC.
“Hata
kwenye mahakama, lazima mtuhumiwa apewe nafasi ya kusikilizwa au kujitetea,
mimi nilikuwa ulingoni na mwamuzi na mpinzani wangu Mchanjo, mwamuzi amenitolea
maneno machafu sana, haikutosha akaamua kunikata pointi, niliandika barua ya
kulalamika TPBC, hawajaniita na kuibuka na adhabu kwangu,” alisema Cheka.
Alisema
kuwa pamoja na uamuzi huo kutomfikia kimaandishi, ameamua kuchukua hatua za
haraka kwani tayari vyombo vya habari mbalimbali na mitandao ya kijamii vimekwishatangaza
uamuzi uliofanywa bila kufuata sheria kwa kumpa nafasi ya kumsikiliza.
Meneja
wa bondia huyo, Juma Ndambile, alisema walichokifanya TPBC ni kumvunja nguvu bondia
wake ili ashindwe kuendelea na mchezo wake.
“Niliwaambia kuwa pambano limeandaliwa na
kampuni inayoitwa Dragon, sasa kwa nini mimi nilipe, pia niliambiwa nitafute
hela ya glovu, niligoma, nadhani hiyo ndiyo imekuwa chanzo,” alisema Ndambile.
Alisema
ili kumpata mshindi sahihi, bora pambano
hilo lilirudiwe ili mshindi apatikane kwa mujibu wa taratibu na siyo kwa njia
iliyotumika ambayo lengo lake ni kuharibu rekodi na kutengeneza ya bondia mwingine.
Awali
juzi TPBC ilitangaza kumfungia Cheka kwa kufanya fujo baada ya pambano
lililofanyika ukumbi wa Vijana Kinondoni kati yake na Mchanjo ambaye
alitangazwa kuwa mshindi.

Comments
Post a Comment