Mwandishi wetu
KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeichapa URA mabao mabao 2-0 katika mchezo wa kirafiki uliopigwa Uwanja wa Phillip Omondi mjini Kampala Uganda.
Azam iko nchini Uganda kwa kambi ya siku 10 ikijiandaa kwa msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).
Kwa mujibu wa habari iliyochapishwa katika tovuti ya klabu hiyo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, alifanya mabadiliko makubwa katika kikosi cha akiwatumia wachezaji wa kikosi cha pili huku walioanza kwenye mechi mbili zilizotangulia akiwapumzisha.
Mabao mawili ya Azam FC yamefungwa na mshambuliaji Yahaya Mohammed, la kwanza akifunga dakika ya 19 kwa shuti kali nje ya eneo la 18 kabla ya kutupia jingine la aina hiyo dakika ya 47.
Mlinda mlango Mwadini Ally, alifanya kazi kubwa kwa kuokoa michomo mingi ya URA.
Katika mchezo uliotangulia Azam ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Uganda KCCA.
Azam FC itacheza mchezo mwingine Jumapili Agosti 13 dhidi ya Onduparaka, mtanange utakaofanyika Uwanja wa Namboole kuanzia saa 10.00 jioni.
Timu hiyo itamaliza ziara yake Jumatatu ijayo kwa kucheza mchezo wa tano wa kirafiki dhidi ya washindi wa tatu wa Ligi Kuu Uganda msimu uliopita, Vipers FC, utakaofanyika Uwanja wa St Marys uliopo Kitende, Uganda.

Comments
Post a Comment