PARIS, Ufaransa
TIMU ya Paris St-Germain imekamilisha dili la kumnunua mshambuliaji wa Brazil, Neymar, kwa ada iliyoweka rekodi mpya ya usajili ya pauni 200 (zaidi ya sh. bilioni 589) akitokea timu ya Barcelona.
Ada hiyo iliyotumiaka kumnunua Neymar inaweza kununua ndege tatu kubwa za abiria aina ya Boeing 737-700 ambapo kila moja inauzwa dola milioni 82.4 (zaidi ya sh. bilioni 184.4) kila moja.
Ada ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 25 imevunja rekodi ya awali iliyowekwa Paul Pogba alipotua Manchester United kutoka Juventus kwa pauni milioni 89 (zaidi ya sh. bilioni 261) Agosti 2016.
Katika mkataba wake atakuwa akilipwa pauni milioni 40.7 (zaidi ya kwa mwaka sh. bilioni 119) kwa mwaka akipata mshahara wa pauni 782,000 (zaidi ya sh. bilioni 2.3) kila wiki, malipo hayo ni kabla ya kulipa kodi katika mkataba wake wa miaka mitano.
Akizungumza baada ya kusaini mkataba Neymar alisema amefurahi kujiunga na moja ya timu kubwa Ulaya".
"Nilikuwa na ndoto kubwa ya kujiunga na Paris St-Germain, pamoja na kujitoleza kwao na nguvu zinazotokana na hili," alisema.
"Najihisi niko tayari kuanza kazi. Kuanzia leo, nitafanya kila niwezalo kuwasaidia wachezaji wenzangu wapya."
Neymar atatambulishwa rasmi kwa mashabiki wa PSG kesho wakati wa mechi yao ya kwanza kabisa ya msimu mpya, ambayo itakuwa nyumbani uwanja wa Parc des Princes dhidi ya Amiens.
Nchini Uhispania, kifungu cha kumwachilia mchezaji kutoka kwa mkataba wake kinaweza tu kufunguliwa kwa mchezaji kulipa pesa yeye binafsi.
Neymar alipofika na pesa Alhamisi kulipa hata hivyo, maafisa wa La Liga walikataa malipo hayo.
Awali kulitokea majibizano kati ya maofisa wa La Liga na wasimamizi wa Ligue 1.
La Liga wanaamini PSG huenda wanakiuka sheria za uchezaji haki kifedha (FFP) kwa kumnunua mchezaji huyo wa Brazil.
Baada ya kushindwa kulipa pesa hizo kwa La Liga, wawakilishi wa Neymar walilipa pauni milioni 200 katika ofisi ya Ofisi za Barcelona FC.
Neymar alijiunga na Barca mwaka 2013 na kushinda nayo mataji mawili ya La Liga na moja la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Aliichezea Barcelona mechi yake ya kwanza dhidi ya Levante Agosti 2013, amefungia mabao 105 na kusaidia ufungaji wa mengine 80 katika mechi 186 .
Alichezea timu ya taifa ya Brazil mara ya kwanza akiwa na miaka18 na kufunga mabao 52 katika mechi 77.

Comments
Post a Comment